SIMBA KUJICHIMBIA VISIWANI ZANZIBAR KWA AJILI YA KUIVUTIA KASI MBAO FC

KIKOSI kamili cha Simba ya jijini Dar es Salaam kitaweka kambi ya mazoezi katika mji wa Zanzibar kujiandaa kwa ajili ya mechi ya Kombe la FA dhidi ya Mbao FC ya Mwanza kwenye uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.

Makamu wa rais wa Simba, Geofrey Nyange “Kaburu” hakupenda kuthibitisha hilo wakati alipoulizwa lakini habari za uhakika zinasema kwamba Simba inakwenda kambini Zanzibar.

"Hatujajua tunaweka kambi wapi, umuhimu ni kwamba tumejiandaa vya kutosha katika mchezo dhidi ya Mbao FC” amesema kaburu.

Lakini chanzo kimoja cha uhakika kinasema kwamba wekundu hao wameamua kwenda kuiwekea Mbao FC kambi maalum Zanzibar kama walivyofanya wakati wanajiandaa kwenye mechi dhidi ya Yanga iliyopigwa Februari 25, mwaka huu na Simba kuibuka na ushindi wa mabao 2-1.

Simba imepania kuifunga Mbao kwa namna yoyote ile ili ipate nafasi ya kushiriki katika michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika (CAF), ikiwa imekosa mashindano ya kimataifa kwa miaka minne sasa.

“Tuakwenda kuiwekea Mbao FC kambi maalum Zanzibar. Hii ni kambi maalum ya ushindi ambayo itakuwa ni kwa ajili ya kwa mechi hiyo,” amesema mtoa habari huyo.

Amasema kwamba wachezaji wote wameambiwa kwamba hakuna wakati wa kufanya mchezo katika mechi hiyo sababu kila mmoja anaitegemea Simba kufanya vyema lakini pia hata nchi zima inawataka Simba.

“Unajua watu wengi wanataka kuona Simba inawakilisha nchi, sasa matumaini haya hayawezi kutimia kama wachezaji hawatajitambua,” amesema.


Simba inefika hatua hiyo baada ya kuiondoa Azam FC kwa bao 1-0 wakati Mbao kwa upande wao waliifunga Yanga kwa idadi kama hiyo ya ushindi.

No comments