SIMBA MGUU SAWA FIFA KUDAI "HAKI" YA POINTI TATU WALIZOPEWA KISHA WAKAPOKWA

MAKAMU wa rais wa Simba, Geofrey Nyange “Kaburu” amesema klabu hiyo ipo kwenye hatua za mwisho za kuwasilisha malalamiko yake katika Shirikisho la Soka Duniani (FIFA).

Akihojiwa na kituo cha redio cha EFM jana, Kaburu amesema kwamba Simba wanakwenda FIFA kudai kile alichosema ni haki ya klabu hiyo na si vingine.

Amesema, alikuwa anasubiri baadhi ya nyaraka kutoka Shirikisho la Soka hapa nchini (TFF), ikiwemo mwenendo wa shauri lao pamoja na uamuzi yaliyofikiwa dhidi ya Kagera Sugar.

Simba walilalamika kwa TFF kuwa Kagera Sugar walimchezesha beki Mohammed Fakhi katika mechi yao iliyochezwa Aprili 2, mwaka huu kwenye uwanja wa Kaitaba akiwa na kadi tatu za njano.

Kamati ya masaa 72 ya Bodi ya Ligi iliipa Simba alama tatu na mabao matatu, lakini baadaye Kamati nyingine ya Sheria, Haki na Hadhi ya wachezaji ikairejeshea Kagera Sugar pointi hizo tatu.

Hata hivyo kamati zote mbili zimekiri kwamba Fakhi alikuwa na kadi tatu za njano jambo ambalo ni kosa kubwa kwa mujibu wa kanuni zinazotawala soka duniani.

Kaburu amesema kwamba TFF wameihakikishia Simba watapewa nyaraka hizo mapema ili waweze kuambatanisha na malalamiko yao katika FIFA.


Baadhi ya wadadisi wa mambo wanasema kwamba kama ikithibitika kuwa Simba wanastahili kupewa alama zao tatu, hukumu ya FIFA inaweza kuiweka katika wakati mgumu TFF kwamba wamekosa waledi katika kuongoza soka.

No comments