SIMBA SC KUMUAGA MWANACHAMA WAO HOSPITALI YA MWANANYAMALA DAR KESHO

UONGOZI wa klabu ya Simba umesema kuwa mwili wa aliyekuwa mwanachama wa klabu hiyo, Shose aliyefariki kwa ajali wakati akitokea Dodoma katika fainali za Kombe la FA ambapo Simba waliwatandika Mbao FC mabao 2-1, utaagwa rasmi kesho.

Akiongea na saluti5, makamu wa rais wa Simba Geofrey Nyange “Kaburu” amesema kuwa mwili wa mwanachama huyo utaagwa kesho saa 5:00 asubuhi, kwenye hospitali ya Mwananyala, jijini Dar es Salaam na misa ya kumuombea itafanyika kanisa la RC, Magomeni.

“Tumepata taarifa kutoka kwa familia kwamba baada ya kukaa pamoja wameamua marehemu Shose atakwenda kuzikiwa Moshi na kulingana na taarifa hiyo, siklu ya Alhamisi itakuwa ni rasmi kwa ajili ya kumuaga,” alisema Kaburu.  

Kaburu amesema kuwa Shose ambaye alikuwa mwanachama wa tawi la “Simba Damu Fans” atasafirishwa kwa njia ya barabara tayari kwa ajili ya maziko Ijumaa hii.

“Marehemu Soshe ni mpiganaji wetu, ni mwanachama wetu ambaye ukweli kabisa msimu huu wa Ligi amekuwa karibu sana na timu, amesafiri karibu maeneo mengi ya Tanzania kuonyesha kuwa yuko bega kwa bega nasi.”

“Tutamkumbuka sana Shose, tulikuwa nae muda wote wa michuano ile ya Mapinduzi Cup kwahiyo kwa hakika ni mtu muhimu sana na amekuwa chachu kubwa sana ya sapoti kwa klabu kupitia tawi lake la Simba Damu Fans,” alisema.

No comments