SIMBA SC YAKUBALI YANGA NI MABINGWA LIGI KUU TANZANIA BARA MSIMU HUU

YANGA ikishinda leo tu dhidi ya Toto African mambo yatakuwa yamekamilika rasmi kuwa mabingwa kwa mara ya tatu mfululizo na kukubalika kwa hilo Simba wamekubali kila kitu wakisema hakuna namna Yanga ndio mabingwa.

Akizungumza Jumamosi mara baada ya mchezo wa Yanga iliyoitandika Mbeya City mabao 2-1, kigogo mmoja wa Simba amesema baada ya matokeo hayo, hakuna namna ubingwa umeonyesha njia ya kutua Jangwani.

Bosi huyo ambaye anasifika kwa msimamo katika klabu hiyo akiwa pia mjumbe wa Kamati ya utendaji, amesema nafasi pekee iliyokuwa imebaki kwao Simba kuweza kutwaa taji ni katika mchezo wa Jumamosi ambao walitaraji Mbeya City ingewazuia Yanga.

Kiongozi huyo ambaye yuko karibu na uongozi wa rais wa Simba, Avens Aveva, amesema wamefanya kazi kubwa ya kuwapa msaada Mbeya City lakini bado mambo yalionekana kuwa magumu.

“Kiukweli hapa tunaweza kusema kuwa hawa wenzetu wameshaukaribia ubingwa. Haya ni makosa yetu wenyewe, hatuna wa kumlaumu, nafasi pekee tuliyokuwa tunaisubiria ni hii ya Mbeya City lakini nayo naona wamepita kwa ushindi,” alisema bosi huyo.

“Tuliwapa msaada wote Mbeya City ili washinde, tukawapa taarifa za kila namna lakini bado walizidiwa akili, hapa hatuna tena nafasi nyingine ndio maana nasema hawa wenzetu watakuwa mabingwa tu, mechi walizobaki nazo ni rahisi.”

Endapo Yanga itashinda leo dhidi ya Toto, watakuwa wamemaliza kazi nzima ya kutwaa taji hilo kwa sherehe za ubingwa kuanza ambapo hakuna timu yoyote itaweza kuizidi kwa pointi, huku ikisaliwa na mchezo mmoja dhidi ya Mbao Jumamosi, Mei 20.    

No comments