SIMBA WAICHEKA YANGA KUSHANGILIA "UBINGWA HEWA" WA LIGI KUU BARA

MASHABIKI wa Yanga wanaamini kwamba timu yao kwa kuifunga Toto Africa ya Mwanza kwa bao 1-0, ni kama wametangazwa mabingwa wa Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara.

Hata hivyo, Simba wamewajibu kwamba kama wanashangilia wajue kuwa wanashangilia “ubingwa hewa” kwasababu Simba kwa sasa inakwenda FIFA kudai pointi zake tatu dhidi ya Kagera Sugar.

Mmoja wa viongozi wa Simba ameiambia saluti5 kwamba dhamira yao ya kukata rufaa FIFA iko palepale na kwamba wiki hii muda wowote rufaa hiyo itatua FIFA.

“Kama Yanga wanashangilia ngoja washangilie kumshusha daraja ndugu yao. Sisi rufaa yetu FIFA tuna uhakika nayo kabisa tukishinda mechi yetu ya Mwadui ndio tutajua nani ni bingwa,” amesema.

Kiongozi huyo amesema kwamba hata kama watashinda dhidi ya Mbao FC na kupata nafasi ya kuiwakilisha nchi katika Kombe la Shirikisho lakini bado hawataacha kulalamikia pointi zao dhidi ya Kagera Sugar.

Simba walikata rufaa kwa bodi ya Ligi kulalamika kwamba Kagera walimchezesha beki wao Mohammed Fakhi akiwa na kadi tatu za njano na Kamati ya saa 72 ikaipa ushindi wa mabao 3 na pointi tatu.

Lakini katika hatua nyingine, TFF kupitia Kamati yake nyingine ya sheria iliwapoka Simba pointi hizo na kuzirejesha kwa Kagera hatua ambayo Simba sasa imewafanya wakate shauri kwenda FIFA.

“Sisi hatujali kama wamepata pointi ngapi tunajua kuwa Ligi bado haijamalizika. Tuna mechi moja dhidi ya Mbao hizo ndizo mechi zitakazoamua ubingwa,” amesema.

No comments