SIMBA YAMREJESHA EMMANUEL OKWI MSIMBAZI... kuzibomoa pia Mbeya City, Azam FC

KUNA vitu anaweza kuonekana kama unafanya haraka kuvisema lakini si dhambi kuzungumzia namna Simba inavyojipanga na msimu ujao.

Saluti5 imefanikiwa kupenye chumba cha siri cha usajili wa klabu ya Simba na kugundua kwamba kuna majina matata yameshatua kwa mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zakaria Hans Poppe.

Kwanza kabisa ni Emmanuel Okwi ambaye anarejea Simba kufanya kazi yake ya mafanikio ambayo amekuwa nayo kwa miaka mingi na kwamba Mganda huyo anasemekana ameshakamilisha kila kitu kuhusu kurejea kwake ndani ya klabu hiyo ya Mtaa Msimbazi.  

Okwi ambaye kwa sasa anacheza katika kikosi cha SC Villa ya Uganda, anakuja kusimama kwenye winga mojawapo ya Simba na nyingine ikimwachia Shiza Kichuya.

Lakini pia jina linguine ambalo linaingia kwenye usajili huo ni nahodha wa Mbeya City, Kenny Ally ambaye amekuwa katika ubora wa hali ya juu katika kikosi cha Mbeya.

Kiungo huyo anacheza kwa kasi kubwa uwanjani na anakuja Simba kuongeza ladha katika nafasi hiyo yenye viungo wengine mahiri.

Lakini pia katika meza ya usajili wa Simba kuna jina la beki matata ambaye pia ni nahodha wa kikosi cha Mbao FC, Yusuph Ndikumana ambaye ukabaji wake unatisha.

Simba imedaiwa kuwa inataka kumsajili beki huyo kufuatia habari kwamba kocha wa timu ya taifa ya Uganda, Micho, amemtafutia timu katika nchi ya Selbia beki wa Simba raia wa Uganda, Juuko Murshid.

Lakini pia katika jalada hilo kuna kiwembe kimoja hatari kutoka klabu ya Nzoia Sugar ya Kenya, Brian Nindo Otieno ambaye ni mmoja wa wapachikaji mabao hodari katika Ligi Kuu ya Kenya.

Simba imedaiwa kuwa imekataa kuwasajili wachezaji wanaotoka Yanga ingawaje kumekuwa na habari kwamba baadhi ya wachezaji hao wamekuwa wakipiga kambi kwenye mlango wa Simba kuomba kusajiliwa.

Lakini pia Simba imedaiwa kutaka huduma ya mmoja wa wachezaji wa Azam FC ambaye hata hivyo jina lake limeendelea kufichwa.

“Haifahamiki kwa nini jina la mchezaji huyo linafichwa, lakini nadhani ni usajili unaongojewa kwa hamu kubwa,” kimesema chanzo chetu.
 

No comments