SIMBA YAZUNGUMZIA KUCHELEWA KWA RIPOTI YA FIFA KUHUSU RUFAA YA POINTI TATU ZA KAGERA

WAKATI ambapo wanachama na mashabiki wa Simba wanasubiri kwa hamu uamuzi wa rufaa ya kudai kupewa pointi tatu za mchezo wa Kagera, uongozi wa wekundu hao umeanika ukweli juu ya suala hilo.

Hivi karibuni Simba ilipeleka ombi katika Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), kudai tafsiri ya kanuni sakata la mchezaji Mohammed Fakhi wa Kagera Sugar aliyetumiwa na tmu yake hiyo huku akiwa ana kadi tatu za njano hivyo hakustahili kucheza.

Kutokana na hali ya sintofahamu iliyojitokeza ndani ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ya kuipa Simba pointi tatu na kisha kuinyima haki ya kupewa pointi tatu, uongozi wa mnyama ulilipeleka sakata hilo FIFA na sasa kunasubiriwa majibu.

Akifafanua juu ya lilipofikia sakata hilo hadi sasa, makamu wa rais wa Simba, Geofrey Nyange “Kaburu” alianika ukweli juu ya lini uamuzi unaosubiriwa na kwamba FIFA wanaendelea kulifanyia kazi lalamiko hilo la kudai haki.

Alisema, pamoja na FIFA kukiri kupokea lalamiko lao, bado kesi yao inashughulikiwa na mahakama ya soka ya dunia (CAS), na maamuzi ya mwisjho yatatumwa kwa TFF pamoja na klabu yenyewe ya Simba.

“Nimelazimika kutoa kauli ya ufafanuzi huu kutokana na kuwepo kwa taarifa za upotoshaji kwamba sakata hilo lingepata majibu yake siku ya Jumanne, jambo ambalo si kweli. Kesi yetu bado imo katika hatua ya kusikilizwa na FIFA na hawakutaja siku ya kutoa uamuzi.”

“Hivyo ninachoendelea kuwaom,ba Wanasimba ni kwamba waendelee kuvuta subira hadi pale FIFA watakapotuma majibu ya kesi tuliyoifungua CAS na sio kweli kuwa majibu yangepatikana Jumanne iliyopita kama walivyovumisha baadhi ya wasioitakia mema Simba.”


“Sisi viongozi tuna mawasiliano ya moja kwa moja na watendaji wa FIFA na kwamba suala letu linashughulikiwa kwa mujibu wa taratibu na kanuni za vikao vya shirikisho hilo ambalo ndilo lenye mamlaka ya mwisho ya masuala ya sheria, kanuni na utaratibu  wa mchezo wa mpira wa miguu duniani,” alifafanua Kaburu.

No comments