NYOTA WA ZAMANI WA YANGA ATUA SINGIDA UNITED

UONGOZI wa klabu ya soka ya Singida United umethibitisha kumsajili mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Atupele Grini wakiwa katika maandalizi ya kuelekea Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara msimu wa mwaka 2017/18.

Akiongea na saluti5, Katibu Mkuu wa Singida United, Abdurahim Sima amesema kuwa si Atupele pekee bali pia kuna wachezaji wengine watatu wa kimataifa kutoka nchini Zimbabwe ambao wameshatua hapa nchini.

“Ni kweli, Atupele yuko kambini tangu juzi na anaendelea kufanya mazoezi akiwa na wenzake wengine,” alisema Katibu huyo.

“Timu yetu imejipanga vizuri kwa kuangalia baadhi ya maeneo yanayohitaji maboresho na kuyafanyia kazi kwa kuwasajili wachezaji ambao tunaona wanahitajika,” aliongeza.

Sima pia amezungumzia tetesi za wachezaji Deus Kaseke wa Yanga na Ibrahim Ajibu wa Simba kutajwa kuwa mbioni kutua katika klabu hiyo ambapo amesema bado hawana mpango nao.

“Mwalimu Hans Pluijim hivi karibuni aliulizwa na waandishi wa habari kuhusu ni wachezaji gani zaidi ambao anaona wanaweza wakafaa kikosini ndipo akawataja Ajibu na kaseke, hayo yalikuwa ni mapendekezo yake tu.”

“Lakini hatujaongea na Kaseke wala Ajibu, kwanza huyo Kaseke mimi hata namba yake sina na hata ukimuuliza atakwambia kuwa hatujazungumza nae lolote.”

Hata hivyo, Sima alisema kuwa bado dirisha la usajili halijafungwa hivyo lolote lionaweza kutokea, ila kwa sasa hawajazungumza na yeyote kati ya Ajibu na Kaseke ingawaje Pliujim ametoa mapendekezo.

No comments