SUNDAY KAYUNI AENDESHA SEMINA YA MAKOCHA KUJADILI MAPUNGUFU LIGI KUU BARA

CHAMA cha makocha Tanzania (TAFCA), kimesema kuwa kinaendelea na mikakati ya kuhakikisha makocha wa Ligi Kuu wanashiriki kozi mbalimbali ili kuweza kuboresha na kujiandaa na Ligi msimu ujao.

Akiongea na saluti5, Katibu Mkuu wa TAFCA, Michael Bundala amesema kwamba tayari makocha wa Ligi Kuu wameshiriki semina yenye lengo la kuangalia ni wapi mapungufu yalijitokeza katika Ligi iliyomalizika hivi karibuni.

Alisema kuwa, semina hiyo imeweza kusaidia kujadili hatua za makusudi kwa ajili ya kuweza kukabili changamoto zilizojitokeza katika msimu na kuweza kujiandaa na msimu ujao.bundala alieleza kuwa semina imeendeshwa na mdau kutoka Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania, Sunday Kayuni ambapo imewawezesha makocha walioshiriki Ligi kutoka klabu zote za soka nchini.

“Kwa kweli tunamshukuru sana Kayuni kwa kukutana na makocha wetu kwa ajili ya kujadili changamoto zilizojitokeza kwa msimu huu na natumaini yamefanyiwa kazi na hayatajitokeza kwa msimu ujao,” alisema Bundala.

Alibainisha kuwa semina hiyo iliwagusa makocha wenye leseni A na B na wameweza kupanga mikakati mbalimbali itakayoweza kuongeza kasi ya maendeleo katika soka hapa nchini.

Pia aliongeza kuwa, TAFCA  itaendelea kufanya tathmini  mbalimbali ya maendeleo ya michezo kwa kuwajengea uwezo waweze kufundisha mchezo huo kwa weledi kwa kufuata kanuni.

No comments