TETESI ZA AISHI MANULA KUSEPA MSIMU HUU ZAIPA AZAM FC "PRESHA PRESHA"

WIMBI la klabu ya Azam FC kukimbiwa na wachezaji wake mahiri kila msimu limezidi kuchukua sura mpya baada ya kuzagaa kwa taarifa za kipa wake tegemeo, Aishi Manula kutaka kuachana na mabingwa hao wa Kombe la Mapinduzi.

Manula ambaye amepewa tuzo ya kipa bora wa msimu amekuwa akihusishwa kutaka kumfuata mchezaji mwandamizi wa klabu hiyo, John Bocco ambaye anasemekana anamalizana na Simba.

Bocco ambaye ni mchezaji mkongwe zaidi kwenye kikosi cha timu hiyo, akiwa mmoja kati ya wachezaji walioipandisha daraja huku pia akiwa na kitambaa cha unahodha, inasadikika ameshasaini makubaliano ya awali na timu ya Simba.

Manula ambaye ni kipa tegemeo wa timu ya taifa ya Tanzania, nae ametajwa kutaka kuachana na timu ya Azam lakini hata hivyo amekuwa akikanusha madai hayo.


“Taarifa zinazonihusisha na Simba hazina ukweli wowote, mkataba wangu na Azam unaelekea ukingoni na sasa tuko kwenye mazungumzo ya kuongeza mwingine,” ilisomeka sehemu ya taarifa iliyotumwa na kipa huyo kwenye akaunti yake ya Instagram.

No comments