TISHIO LA MVUA LAPEKEA DAR LIVE KUFUTA ONYESHO LA CHRISTIAN BELLA LEO USIKU


Onyesho la Mfalme wa masauti Christian Bella lililokuwa lifanyike leo usiku ndani ya ukumbi wa Dar Live, Mbagala, limefutwa kwa hofu ya mvua.

Mashabiki wa Mbagala na vitongoji vyake walikuwa wanamsubiri kwa hamu kubwa Christian Bella baada ya kuadimika ukumbini hapo kwa takriban mwaka mzima.

Bella akiwa na bendi yake ya Malaika, ilikuwa ashuke na nyimbo mpya kabisa ukiwemo “Shuga Shuga” ambao bado haujasikika popote pale Dar es Salaam.

Mwimbaji huyo ambaye hivi karibuni alikuwa na ziara ndefu nje ya nchi, angesindikizwa na wadada wawili hatari kwa kushambulia jukwaa - Pam D na Gigy Money pamoja na wasanii wengine kibao.

Mratibu wa onyesho hilo, Juma Mbizo ameiambia Saluti5 kuwa kutokana na tishio la mvua, pande zote zinazohusika na show hiyo, zimekubaliana kwa kauli moja kuahirisha tukio hilo kubwa la burudani.

Mbizo amesema onyesho hilo litapangiwa tarehe nyingine baada ya mapumziko ya mwezi mtukufu wa Ramadhan.

“Kutokana na ratiba ya Bella kwenda kutumbuiza nyumbani kwao Congo pamoja na kujaa kwa kalenda ya maonyesho yake, hukutakuwa na nafasi nyingine kwake kabla mwezi mtukufu wa Ramadhan,” alisema Mbizo.

No comments