TUSA YAENDELEA KUWAPIKA WANARIADHA WATAKAOSHIRIKI MASHINDANO YA VYUO VIKUU VYA DUNIA

SHIRIKISHO la michezo la vyuo vikuu nchini (TUSA), linaendelea kuwaandaa wanariadha wawili waliopata fursa ya kwenda kushiriki katika mashindano ya 29 ya vyuo vikuu vya dunia.

Mashindano hayo yatakayowashirikisha wanamichezo kutoka vyuo vikuu mbalimbali duniani yanatarajiwa kufanyika Agosti 19 hadi 30, mwaka huu katika mji wa Taepei nchini China.

Haya yamebainishwa na Katibu mkuu wa TUSA, Noel Kiunsi alipozungumza na waandishi wa habari hivi karibuni juu ya maandalizi hayo.

Alisema kuwa kwa sasa wanafanya mazoezi katika vyuo vyao ambapo baadaye kutakuwa na pogramu maalum ya kuweka kambi ya pamoja ya kocha ambaye atasimamia maandalizi ya wanariadha hao.

Kiunsi alisema kuwa mashindano hayo yatakutanisha wanaridha kutoka vyuo mbalimbali duniani ambayo ndiyo yatakayotoa mabingwa wa riadha wa umbali tofauti na dunia.

Kiunsi aliwataja wanariadha hao kuwa ni Happy Mahamudu kutoka chuo kikuu cha kilimo cha sokoine (SUA) na Taratibu Machaku kutoka chuo kikuu Dar es Salaam (UDSM), ambao wapo chini ya udhamini wa shirikisho la vyuo vikuu duniani.

“Tunatamani kushirikisha wanamichezo wengi wawe wanashiriki lakini changamoto iliyopo ni fedha ila tunashukuru hawa wawili safari yao inadhaminiwa na shirikisho la dunia hadi watakapofika eneo na mashindano na mpaka yatakapomalizika,” alisema Kiunsi.


Alifafanua kuwa kwa sasa wanaridha hao wanafanya mazoezi yao lakini watakutana ili kuweka kwenye kambi pamoja  na kufanya maandalizi chini ya kocha.

No comments