TWANGA PEPETA: HATUJAMSIMAMISHA CHOCKY, TUMEMPA MUDA WA KUMALIZA ‘VIMEO’ VYAKE


Mkurugenzi wa Twanga Pepeta, Asha Baraka ameiambia Saluti5 kuwa hawajamsimamisha kazi Ally Chocky bali wamempa likizo ya bila malipo ili amalize kazi zake za nje ya bendi.

Akiongea na Saluti5 kwa njia ya simu jana jioni, Asha Baraka akasema maonyesho ya Chocky nje ya Twanga Pepeta yamekuwa yakija kwa wingi na bila mpangilio maalum hivyo kuithiri bendi kwa namna moja au nyingine.

Asha Baraka amesema kutokana na hali hiyo wameamua kumpa Chocky likizo ya miezi miwili bila malipo ili amalize viporo vyake vya kile anachokiita ‘ziara ya miaka 30 ya Ally Chocky kwenye game ya muziki wa dansi’.

Saluti5 ilipomuuliza iwapo atakuwa tayari kumrejesha Chocky kazini pindi akisema amemaliza maonyesho yake,  Asha Baraka alisema: “Hata leo akisema amemaliza tutamrejesha kazini.

“Akituandikia barua kueleza kuwa amemaliza maonyesho yake na hatafanya hivyo tena hadi atakapomaliza mkataba wake, hatutakuwa na tatizo.

 “Hata kama ni baada ya hiyo miezi miwili, bado pia tutahitaji atuthibitishie kwa maandishi kuwa sasa amemaliza maonyesho yake.”
Chocky alipoulizwa na Saluti5 juu ya kauli ya Asha Baraka, alisema hayo ni maendeleo mapya lakini anachojua yeye ni kuwa kasimamishwa kazi kwa miezi miwili.

“Meneja wa bendi Hassan Rehani alinitumia meseji kunitaarifu kuwa nisiende kazini hadi nitakapofahamishwa na nilimpompigia simu kuhitaji ufafanuzi aliniambia nimesimimishwa hadi tarehe 1 Julai na barua ya kusimamishwa imeshaandikwa,” anaeleza Chocky.

Chocky akaimbia Saluti5  kuwa bado ana maonyesho mawili, moja lipo mwezi huu na lingine litafanyika aidha mwezi Juni mwishoni au Julai mwanzoni.

“Niko vizuri na boss wangu Asha Baraka wala wapenzi wasiingie shaka kuna mambo mazuri yanakuja ndani ya Twanga Pepeta,” alisema Chocky bila kufafanua.
No comments