TWANGA YAMUOMBA THABIT ABDUL AKAWAPIGIE GITA LA BASS ALHAMISI USIKU …ni baada ya wapiga bass wao kupata dharura


Mkali wa kinanda na kiraka wa vyombo vingi vya muziki wa dansi na taarab, Thabit Abdul yuko kwenye jukwaa la Twanga Pepeta akisaidia kupiga gitaa la bass.

Alhamisi usiku Twanga wako katika ukumbi wa Monie Junction (Kwa Jimmy) huko Lumo ambako gitaa zito la bass litakuwa likingurumishwa na Thabit Abdul.

Thabit ameiambia Saluti5 kuwa ni kweli anakwenda kusaidia kupiga bass la Twanga baada ya kuombwa na kiongozi wa bendi hiyo Luizer Mbutu.

“Luizer alinipigia na kuniambia leo wapigaji wao wana dharura, hawana mtu wa bass na hivyo kunitaka nikaisaidie bendi yangu ya zamani. Sikuwa na kipigamizi,” alisema Thabit na kusema Twanga ni kama nyumbani.

Jana Thabit Abdul alichafua hali ya hewa mitandaoni baina yake na Twanga baada ya kutoa shutuma kubwa kwa bendi hiyo kwa kufunika bango la kundi lake la Wakali Wao katika ukumbi wa Mango Garden.

Hata hivyo, kitendo cha Twanga kumwita kwenda kuokoa jahazi siku moja tu baada ya mtafaruku wao na  hatua ya Thabit kuitikia wito huo, kunaonyesha kuwa  udugu baina ya pande hizo mbili bado uko imara.

Pichani juu ni picha ya maktba yetu ikimuonyesha Thabit Abdul akiwa Asha Baraka kwenye show ya Twanga Pepeta wiki mbili zilizopita ndani ya Mango Garden Kinondoni.

No comments