VITA YA KUSHUKA DARAJA YAZIWEKA ROHO JUU MAJIMAJI, NDANDA NA TOTO AFRICA

VITA ya kushuka daraja kwenye michuano ya Ligi Kuu Bara imepamba moto ambapo timu zote zilizo kwenye hatari ya kuteremka zimebakiza wastani wa mechi moja kabla ya mzunguuko huu wa pili kukamilika.

Timu ya JKT Ruvu kusalimika ni vigumu kama ngamia kupenya kwenye tundu la sindano, wakati Majimaji, Toto Africa, Ndanda na Mbao zinapaswa kupigana mara mbili zaidi ya uwezo wake ili kubaki salama.

Mtifuano wa timu hizo zinazokamata nafasi ya chini kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara ni mkubwa kuliko ule wa Simba na Yanga ambao wanawania ubingwa msimu huu.

JKT Ruvu wanakamata nafasi ya mwisho wakiwa na alama 23, majimaji wao wana pointi 29 sawa na Toto Africa wakati Ndanda walikuwa na pointi 30 kabla ya mchezo wa wikiendi iliyopita, sawa na Mbao FC ya jijini Mwanza.


Katika mchujo huo, zinashuka jumla ya timu tatu kwenda Ligi daraja la kwanza ambayo ina ushindani mkubwa na kuzipisha timu zilizopanda ambazo ni Njombe Mji, Lipuli FC ya Iringa na Singida United inayonolewa na kocha wa zamani wa Yanga, Hans Pluijim.

No comments