WACHEZAJI MPIRA WA MIGUU WAHIMIZWA KUJIUNGA NA SPUTANZA

WACHEZAJI mpira wa miguu nchini wamehimizwa kujiunga na chama cha wachezaji nchini (SPUTANZA), ili kujiweka ndani ya umoja na pia kufaidika na manufaa yatokanayo na chama hicho.

Mwenyekiti wa SPUTANZA, Mussa Kissoky alisema kuwa kuhimizwa kwa wachezaji kunatokana na umuhimu wa kuwasimamia wanandinga hao pindi wanapohitaji kusaidiwa wanapopata matatizo.

Alisema chama chao ndicho chenye wajibu wa kuwaunganisha wanasoka nchini sambamba na kuwasaidia katika matatizo ya kimikataba na migogoro ya ndani ya klabu ama timu wanazozitumikia.
“Ikiwa wachezaji watakuwa wanachama itatusaidia sana sisi kama chama kuhakikisha tunasimamia haki za wachezaji zinapatikana na kuondoa migogoro hapa nchini baina ya wachezaji na klabu kuhusu masuala ya mikataba yao iweze kubakia historia hapa nchini,” alisema.


Aliongeza kuwa hivi sasa chama kimeandaa mkakati wa kuhakikisha suala la uanachama kwa wachezaji wanaoshiriki Ligi za shirikisho liandikwe katika kanuni ili kutoa nafasi kwa mchezaji kuwa mwanachama.

No comments