WACHEZAJI SIMBA WAZIPANIA MWADUI NA MBAO FC

KIKOSI cha Simba kinaendelea kujifua kwa ajili ya kumaliza Ligi Kuu Tanzania Bara kwa mechizya mwisho dhidi ya wachimba madini wa Mwadui na ile ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Mbao.

Katika mazingira ya kupania kufanya vyema na kuibuka na ushindi, wachezaji wote wamejilisha kiapo cha kucheza kufa na kupona ili kupata pointi tatu ambazo ni muhimu kwa ajili ya kuamua mustakabali wa ubingwa wa msimu huu na ile ya Shirikisho dhidi ya Mbao.

Wakiongea na saluti5, wachezaji waliozungumza kwa niaba ya wenzao walikiri kwa kauli moja kwa kusema “Mechi hiyo ni sawa na fainali hivyo ushindi ni lazima.”

Nahodha wa kikosi cha wekundu hao, Jonas Mkude  alikuwa wa kwanza kuuzungumzia mchezo huo na kujillisha kiapo kwa kusema matokeo ya mechi zilizopita ni chachu ya kufanya vyema katika mechi ya mwisho dhidi ya Mwadui.

“Tumepata somo katika mechi zilizopita, tunataka kuona tunapata mafanikio yatakayoifanya Simba ijiweke katika nafasi nzuri ya kuamua nani anatwaa ubingwa wa Tanzania bara,” alisema Mkude.

Kiungo Muzamiru Yassin kwa upande wake alizungumzia namna timu inavyohitaji ushindi kama ilivyokuwa katika mechi zote zilizopita.

“Tunachohitaji sasa ni kuona timu inapata matokeo mazuri katika kila mechi kuanzia ile ya Mwadui na kisha ushindi dhidi ya Mbao FC katika fainali za FA,” alisema Muzamiru.

Naye Laudit Mavugo alisema “Yaliyopita ni kama hamasa ya mchezo, lazima tuyagange ya baadaye kwa kusaka ushindi kwa udi na uvumba katika mechi mbili zijazo na Mwadui na Mbao.”


“Tutacheza kwa kusaka ushindi mwanzo mwisho kuanzia katika mechi hii dhidi ya Mwadui ambayo pamoja na ugumu wake inatulazimu kucheza kufa na kupona ili tupate pointi tatu muhimu,” alisisitiza beki kiraka James Kotei.

No comments