YANGA YAIPIGA BAO SIMBA SC UDHAMINI WA SPORTPESA

YANGA wanaonekana kuwa na akili sana. Tayari wameshasaini mkataba wa udhamini na kampuni ya Sportpesa na wakaipiga bao haraka Simba kwa kupata mabilioni zaidi ya wekundu hao.

Taarifa kutoka ndani ya yanga ni kwamba Yanga imesaini mkataba huo mnono utakaotangazwa kesho Jumanne makao makuu ya klabu hiyo, ni kwamba yanga itavuna kiasi cha sh. mil 950 kwa mwaka, kiasi ambacho ni kikubwa kidogo kulingana na kile cha Simba.

Katika mkataba wa Simba, klabu hiyo inaonyesha itachukua kiasi cha sh. mil 880 kwa mwaka mmoja na kufanya kwa miaka mitano, Simba itavuna kiasi cha sh. bil 4.

Yanga mbali na hilo, pia itajiwahia mamilioni zaidi mapema mara baada ya kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu bara ambapo itachukua kiasi cha sh. mil 100 ikiwa ni zawadi baada ya kuwa bingwa ikiwapiga bao Simba.

“Unajua sisi tuna tofauti kubwa na Simba, wao wamesaini mkataba ambao watachukua sh. mil 880 kwa mwaka, lakini Yanga tutachukua zaidi ya hapo kwa mwaka. Tutachukua kiasi cha sh. mil 950,” kilisema chanzo kimoja.


“Tulilazimika kukomaa na hawa jamaa kwa kuwa sisi Yanga tuna timu tofauti, kwanza ukiangalia hawa wenzetu hawajashiriki mashindano ya kimataifa kwa muda mrefu lakini rekodi yetu Yanga ni nzuri katika eneo hilo.”

No comments