YOUTHE ROSTAND AHESABIWA SEKUNDE KUDONDOKA JANGWANI

YANGA inataka kufanya usajili wa nguvu na kwamba kwa sasa wako katika mazungumzo ya mwisho ya kumalizana na kipa raia wa Cameroon, Youthe Rostand.

Taarifa kutoka ndani ya Kamati ya usajili ni kwamba vigogo hao wameshakutana na Rostand ambaye kikosi chake cha African Lyon kimeshuka daraja ambapo kipa huyo ameshakubali kila kitu.

Bosi huyo amesema kinachosubiriwa kwa sasa ni wakala wa mchezaji huyo kutua nchini ili wamalize usajili huo ambapo sasa Yanga imemficha katika moja ya hoteli za jijini Dar es Salaam kipa huyo mrefu.

Aliongeza bosi huyo kwa kusema kuwa endapo usajili wa kipa huyo utakamilika, huenda ukawa mwisho wa kipa mkongwe Ally Mustapha “Barthez” ambaye kiwango chake kimeonekana kuanza kushuka akishindwa kuwapa changamoto wenzake Benno Kakolanya na mkongwe mwingine Deogratias Munishi “Dida”.

“Tunataka kumchukua yule Rostand, kila kitu kimeshakaa sawa na hakuna wasiwasi tumezungumza nae na kimsingi amemaliza mkataba wake na klabu yake ambayo nayo imeshuka daraja,” alisema bosi huyo.


“Mawasiliano na wakala wake tumeyafanya, kuna mambo tumeshakubaliana na sasa tunasubiri ili aje nchini tumalize hii biashara. Akija hapa yule kipa atatusaidia sana, tunataka kujenga timu imara kuelekea mashindano ya msimu ujao.”

No comments