ABDI BANDA, AJIBU WAZUA "SINTOFAHAMU" SIMBA SC

KLABU ya Simba ya Dar es Salaam imesema kwamba imetimiza wajibu wake kama klabu kwa kufanya mazungumzo na wachezaji wake wanaomaliza mikataba.

Kiongozi mmoja wa wekundu hao amesema kwamba Simba imetimiza wajibu wake kwa kufanya mazungumzo na wachezaji wote ambao mikataba yao inamalizika na wote wamekubali kusaini mikataba mipya.

“Ni kweli kwamba kuna wachezaji mikataba yao inamalizika lakini wote hao wamefanya mazungumzo ya awali na tumekubaliana. Kama kuna mtu leo anaaga kwamba anaondoka ni uamuzi wake lakini kama Simba tungependa kuendelea na kila mchezaji ambaye tuliongea naye,” amesema kiongozi huyo.

Kiongozi huyo amesema kwamba ameshitushwa na hatua ya mchezaji mmoja, Abdi Banda kuanza kuwaaga mshabiki kwamba anaondoka wakati anajua kwamba yuko kwenye mazungumzo ya kuongeza mkataba.

“Pengine hataki tena kuichezea Simba. Sisi kama uongozi tumetimiza wajibu wetu. Tuko katika mchakato wa kusaini mkataba mpya. Sasa kama anaaga ngoja tuone mwisho wake,” amesema.

Pamoja na Abdi Banda kueleza anakwenda nchini Afrika Kusini kucheza soka la kulipwa, taarifa za uhakika kutoka ndani ya Simba zinaeleza tayari Banda na uongozi wa Simba walishazungumza.

“Banda alizungumza na uongozi kuhusiana na usajili wake na walikubaliana vizuri kabisa.

Kilichokuwa kimebaki ni suala la usajili tu. Sasa inashangaza kama utasikia kuwa ameamua kuondoka,” amesema kiongozi huyo.

Juzi Banda aliandika kwenye ukurasa wake wa Instagram akiwaaga mashabiki wa Simba baada ya kuwa ameichezea mechi ya fainali ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Mbao FC na Simba kubeba ubingwa, hatua ambayo ilijibiwa na mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zakaria Hans Poppe.

Mwenyekiti huyo alisema kwamba hafurahishwi na tabia hiyo kwasababu Banda bado ana nafasi ya kuongeza mkataba katika Simba.

Mchezaji mwingine anayedaiwa kuwa alikuwa akitangaza yuko huru wakati ameshafanya mazungumzo ya kusaini mkataba ni Ibrahim Ajib na viongozi wa Simba wameshangazwa na hatua hiyo.

Ajib anadaiwa kuwa anataka kusajiliwa na Singida United na pia huku Yanga wakiwa wanamtaka.

Hata hivyo kiongozi huyo amesema kwamba safari hii Simba haitamlazimisha mchezaji yeyote kubaki katika kikosi chake.


“Kuna wakati tulimbembeleza sana Hassan Kessy hapa akawa anagoma nasi tukamdekeza lakini mambo aliyotufanyia baadaye kila shabiki wa Simba ameyaona,” amesema.

No comments