ABRAMOVICH AMPA JEURI YA USAJILI ANTONIO CONTE ... Lukaku, Tiemoue Bakayoko njiani kutua Stamford Bridge


KULIKUWA na taarifa katika siku za karibuni kwamba hali si shwari kati ya mmiliki wa Chelsea, bilionea Roman Abramovich na kocha Antonio Conte, lakini sasa mambo yamewekwa sawa na klabu hiyo imekubali kumpa bajeti ya pauni milioni 250 kusajili mastaa anaowataka kiangazi hiki.

Conte alielezwa kukerwa na hatua ya bodi ya klabu kumwekea ngumu kumpa fedha za kusajili wachezaji anaowataka ili kuimarisha kikosi chake kwa msimu ujao.

Straika wa Everton, Romelu Lukaku na kiungo wa ulinzi Tiemoue Bakayoko wa Monaco wanatarajiwa kukamilisha dili Stamford Bridge wakati wowote kutoka sasa, huku beki wa kati Leonardo Bonucci na beki wa kushoto Alex Sandro wote kutoka Juventus wakiwa kwenye rada.

Tayari Mtendaji Mkuu wa Juventus, Giuseppe Marotta, amethibitisha kukataa ‘ofa nono’ ya Chelsea kwa ajili ya Sandro, lakini akaliambia gazeti la Correire della Sera kuwa wanaweza kufeli nia yao ya kutaka kumbakisha kwani siku hizi wachezaji ndio wenye uamuzi juu ya mustakabali wao.

Chelsea inahitajika kuvunja rekodi yake ya uhamisho kufanikisha kumpeleka beki huyo wa miaka 26 Stamford Bridge, kutokana na ukweli kwamba Juventus imemthaminisha kwa dau kubwa la pauni milioni 55.

No comments