AFRICAN MINOFU KUKINUKISHA GARDEN BREEZE EID EL FITR

AFRICAN Minofu Band iliyo chini ya nguli wa muziki wa dansi nchini, Matei Joseph wanatarajiwa kutoa burudani kali ya Eid el Fitr ndani ya kiwanja cha Garden Breeze siku ya Idd Mosi.

Garden Breeze iliyocharuka upya hivi sasa baada ya kuonekana kupoteza mwelekeo kipindi cha kati, inatarajia kuwaka moto kuanzia kwenye Sikukuu ya Eid el Fitr na kuendelea ambapo burudani itakuwa ikirindima kila uchao.

Matei ameiambia saluti5 kuwa, kikosi chake kimejipanga vilivyo kuhakikisha anakata kiu ya mashabiki wake waliyokuwa nayo kwa takriban mwezi mmoja sasa tangu kuingia kwenye mfungo mtukufu wa Ramadhani.

“Nawaombamashabiki wetu wote wafike kwa wingi siku hiyo kwani burudani itaanza mapema zaidi na kuendelea hadi majogoo,” amesema mkali huyo wa uimbaji na kucharaza Drums.


Amesema kuwa, bendi yake inayokusanya wanamuziki wengi mahiri na wakongwe, inaahidi kumimina dansi la kukata na shoka ikiwa ni pamoja na vibao vyao vipya ambavyo ni maandalizi ya albamu yao ijayo.

No comments