ANDRE SILVA "AIBOMOA" MANCHESTER CITY BAADA YA KUTUA AC MILAN

FUJO za usajili wa wachezaji haipo hapa Tanzania tu ambapo watu wanatongoza wachezaji, lakini wakigeuka tu wengine wanakuja kuwabeba kirahisi.

Kuna klabu kadhaa duniani zimeamua kutumia umafia wa hali ya juu katika kusajili wachezaji wanaowataka na huwa hawashindwi kitu.

Kati ya klabu zinazofanya balaa kubwa msimu huu wa usajili ni AC Milan ya Italia ambayo inaonekana imepania kurudisha heshima yake iliyopotea kwa miaka kadhaa sasa kwa kununua wachezaji wakubwa.

Katikati ya wiki klabu hiyo ilitawala vichwa vya habari baada ya kununua mmoja wa washambuliaji waliokuwa wakisakwa na klabu nyingi msimu huu, Andre Silva.

Nyota huyo ambaye alikuwa akisakwa kwa karibu zaidi na klabu ya Manchester City, ameamua kuikacha klabu hiyo ya Uingereza na kuamua kwenda AC Milan kwa dau la euro mil 38 akitokea klabu ya FC Porto ya Ureno.

Alipoulizwa kwanini ameamua kuachana na dili la Man City, Silva amesema kwamba ni kama matajiri wa klabu hiyo ya Uingereza hawakuwa “siriazi” katika usajili huo.

“Kweli tulizungumza lakini hawakuwa kama wanataka kweli nikasajili kwao. Unajua katika wakati wa usajili kila timu ina mbinu zake za kusajili, wengine ni maneno matupu,” amesema katika hali inayojitafsiri kama ni kuiponda Man City.

“Hata hivyo nawaheshimu sana na wakati mwingine tunaweza kuzungumza, lakini kwa sasa akili yangu imehama, haipo kwao kabisa,” amesema.

Msimu ulioisha Silva alifunga jumla ya mabao 20 katika michezo ya Ligi Kuu Ureno pamoja na ile ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, huku timu ya taifa akifunga mara 17 na kusaidia mara saba katika michezo 33.

Kocha wa Man City, Pep Guardiola alipoulizwa kuhusu suala hilo alisema kwamba kila mchezaji anakwenda kwenye timu anayoipenda.


“Ni kweli tulikuwa tuna haja nae, lakini kama amekwenda AC Milan huko ndiko kwenye mapenzi makubwa kwake, sina la zaidi.”

No comments