BAJETI YA LIPULI FC MSIMU UJAO USIPIME... zaidi ya sh. mil 800 zahesabiwa siku kutua klabuni

UONGOZI wa klabu ya Lipuli kutoka Iringa umetangaza bajeti yake itakayotumika katika msimu ujao wa Ligi kujiweka kwenye malengo ya kumaliza katika nafasi mbili za juu kwenye msimamo.

Mwenyekiti wa klabu hiyo kutoka nyanda za juu kusini mwa Tanzania ambayo imefanikiwa kupanda daraja kucheza Ligi Kuu katika msimu wa mwaka 2017/18, Abdul Majeki amesema wana mpango wa kupata udhamini kutoka kwenye makampuni makubwa mbalimbali.

“Kwa hesabu ya haraka haraka ni kwamba kuna zaidi ya sh. mil 800 ambayo tutaitumia, lakini hadi sasa Kamati ya Mipango, Uchumi na Fedha ina taarifa kuwa kama mungu atatujalia, kuna kampuni tatu kubwa ambazo zimeonyesha nia ya kuingia mkataba na sisi katika udhamini mbalimbali,” alisema.

“Kwahiyo tunategemea kati ya Jumamosi na Jumapili wiki hii tutaingia mkataba na kampuni mojawapo ili kutudhamini kwa muda wa miaka miwili.”

“Tumepania kuipanga timu kikamilifu ili tukashindane Ligi na kwenda kushiriki tu, hatuna lengo la kuingia kushiriki na baadae kushuka bali tunafikiria kupata nafasi mbili za juu.”

“Hii ni timu ya primier ligue, lazima tuwe na fungu la kutosha kwa ajili ya kutengeneza benchi zuri la ufundi, kusajili vizuri, uweze kuwahudumia wachezaji vizuri pamoja na kuwalipa vizuri haki zao tulizokubaliana.”


“Tuna imani bajeti ya mil 800 inaweza ikatusaidia vizuri zaidi kwasababu tuna mpango wa kununua basi, kutafuta hosteli kwa ajili ya wachezaji kwahiyo ni mambo ambayo tuna imani tutafanikiwa kulingana na malengo tuliyojiwekea,” alisema.

No comments