CHAMA CHA NGUMI DAR CHAKUMBWA NA UHABA WA ULINGO

CHAMA cha ngumi za ridhaa mkoa wa Dar es Salaam (DABA), kinasema kuwa kinakabiliwa na ukosefu wa ulingo wa mkoa kwa ajili ya kufanyia maandalizi kwa timu ya mkoa katika kujiandaa na mashindano mbalimbali ya ndani na nje ya nchi.

Katibu mkuu wa DABA, Wamboi Mangore alisema kuwa ukosefu wa ulingo wa mkoa unachangia kwa timu ya mkoa kufanya mazoezi katika hali ngumu wakati ikijiandaa na mashindano ya kitaifa na kimataifa.

Alisema kuwa changamoto nyingine ni pamoja na vifaa vya michezo kwa timu ya mkoa ambayo huchaguliwa kupitia mashindano kwa ajili ya kujiandaa na mashindano mbalimbali.

Mangore alisema kuwa mahitaji hayo yanahitajika ili timu ya jiji iweze kuandaliwa vyema na iweze kwenda kuiwakilisha vyema nchi katika mashindano ya ndani na nje ya nchi.

“Hizi ni miongoni mwa changamoto ambazo zinatukabili kama chama, hivyo tunaomba wadau kutuunga mkono katika kutuwezesha kuendeleza michuano kutokana na Dar es Salaam ndio kitovu cha michezo hii,” alisema Mangore.

Akizungumzia mashindano ya majiji yaliyomalizika hivi karibuni, alisema chama kinaipongeza timu ya MMJKT kwa kutwaa Kombe la mashindano ya Mstahiki Meya wa jiji la Dar es Salaam kwa mara ya nne mfululizo tangu kuanzishwa kwake.

Alisema kuwa timu hiyo imetetea ubingwa na Kombe baada ya kupata medali nne za dhahabu ikifuatiwa na mshindi wa pili timu ya Magereza iliyopata medali mbili za dhahabu na ya tatu ni timu za Mombasa Count na Kigamboni zilizopata medali moja moja ya dhahabu. 

No comments