CHELSEA YAKWAMA KWA MARCO VERRATTI WA PSG


CHELSEA inaonekana dhahiri kushindwa jaribio la kutaka kumchukua kiungo Marco Verratti wa Paris Saint-Germain kiangazi hiki, ambaye  amewaambia marafiki zake wa karibu kuwa yuko tayari kujiunga na Barcelona ambayo inaelezwa tayari imeweka mezani ofa ya pauni milioni 88.

Kiungo wa zamani wa Barca, Xavi ambaye kwa sasa anaichezea Al Sadd ya Qatar ameripotiwa kuishauri klabu yake hiyo ya zamani kutumia kiasi chochote cha fedha kumsainisha  Verratti kiangazi hiki akiamini ndiye mtu sahihi wa kurejesha ubora wa kiungo uliofifia Nou Camp tangu alipoondoka 2015, huku Andres Iniesta umri ukimtupa mkono.

Kwa mujibu wa gazeti la Calciomercato, mkataba tayari umeingiwa baina ya timu hizo mbili, wakati Mundo Deportivo limeripoti kwamba Verratti alikuwa ameelekeza moyo wake kujiunga na Barcelona tangu timu hiyo ilipoitupa nje PSG katika Ligi ya Mabingwa Ulaya Machi mwaka huu.


Kocha wa Chelsea, Antonio Conte ameripotiwa kujiamini kumuhamishia Stamford Bridge Mtaliano huyo mwenzake kiangazi hiki, lakini tetesi zilizopo sasa zinabainisha ufinyu wa lengo hilo kutimia.

No comments