EMMANUEL OKWI ASEMA SIMBA ANAYOIONA SASA NDIO ANAYOITAKA

KIUNGO mshambuliaji wa kimataifa, Emmanuel Anord Okwi raia wa Uganda, amesema Simba anayoiona sasa ndio ile anayoitaka yeye na anaamini uwepo wake utaleta chachu kubwa na Simba itakuwa timu tishio barani Afrika.

Tayari Mganda huyo ameshamalizana kila kitu na Simba SC kufuatia mwenyekiti wa kamati ya usajili wa mabingwa hao wa Kombe la FA, Kapteni mstaafu wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Zacharia hans Poppe kumfuata hukohuko Uganda.

Hans Poppe amfuate Okwi nchini Uganda hasa baada ya kusikia minong’ono ya hapa na pale kuwa huenda mshambuliaji huyo wa zamani wa Yanga na Etoile Du Sahel akanaswa na klabu moja ya nchini Senegal.

Hata hivyo, Okwi amesemekana kufurahi kukutana na Hans Poppe na kuamini kuwa Wanasimba wanamkubali, hivyo akaona ni bora arejee mitaa ya Msimbazi, Kariakoo, jijini Dar es Salaam.

Nyota huyo inadaiwa amesaini mkataba wa miaka miwili ambapo atasalia Msimbazi hadi mwaka 2019.
Okwi alifurahishwa na kikosi cha Simba, hasa baada ya kusikia majina kama Shomary Kapombe, John Bocco “Adebayor”, Shiza Kichuya, Laudit Mavugo na Jonas Mkude.

Mshambuliaji huyo wa timu ya taifa ya Uganda “The Cranes” alijiunga na Simba mwaka 2010 akitokea SC Villa ya Uganda ambako ndiko alikoanzia soka lake la ushindani.


Okwi aliuzwa Tunisia na kujiunga na Etoile Du Sahel ambako alijiunga na Yanga mwaka 2014, kabla hajarejea tena Simba mwaka 2015. 

Aliuzwa tena nchini Denmark na klabu yake ya Simba kwa klabu ya Sonderjsky inayoshiriki Ligi Kuu nchini humo na mwaka huu anarejea tena Msimbazi akitokea SC Villa ya nyumbani kwao Uganda ambayo ilimpokea baada ya kuachana na timu hiyo ya Denmark.

No comments