FM ACADEMIA KULA IDD BILA NYOSHI …bendi mpya yanukia


FM Academia “Wazee wa Ngwasuma” itaangusha show za Idd el Fitr bila ya aliyekuwa rais wao Nyoshi el Saadat ambaye ni kama vile ameipa kisogo bendi hiyo.

Habari za uhakika zilizofikia Saluti5 ni kwamba Nyoshi ameamua kukaa kando kwanza kabla ya kuamua kuendelea na bendi au la.

Idd Mosi FM Academia watakuwa BL Park Tabata Segerea na Idd Pili watapatatikana Bulyaga Bar, Temeke.

Kujiweka kando kwa Nyoshi kulithibitika jana ambako hakuibuka kwenye onyesho la bendi hiyo lililofanyika Monie (Kwa Jimmy) na leo usiku pia anatarajiwa kukosekana katika show itakayofanyika Tegeta ndani ya ukumbi wa Brazil Pub.

Juzi FM Academia ilifanya mabadiliko ya uongozi kwa kumvua urais Nyoshi el Saadat na kumpa nafasi hiyo Patcho Mwamba.

Rais huyo mpya wa FM Acedemia amekiri kuwa Nyoshi ameweka wazi kwamba hawezi kuongozwa na yeye (Patcho) hali inayoashiria kuwa ‘ndoa’ ya Nyoshi na FM Academia imefikia ukingoni.

Saluti5 imepenyezewa habari za ndani kuwa bendi mpya itazaliwa ubavuni mwa FM Academia kupitia mabadiliko hayo ya uongozi.

No comments