FM ACADEMIA YASITISHA ‘UFALME’ WA NYOSHI …Patcho Mwamba rais mpya wa bendi


Hatimaye FM Academia imefanya mabadiliko ya uongozi ambayo yanamnyofoa Nyoshi el Saadat kwenye cheo cha urais na sasa anakuwa mwanamuziki wa kawaida.

Nafasi ya Nyoshi inarithiwa na mwimbaji mzoefu Patcho Mwamba ambaye anahitimisha takriban miaka 20 ya urais wa Nyoshi katika bendi hiyo.

Msemaji wa FM Academia Kelvin Mkinga ameithibitishia Saluti5 juu ya mabadiliko hayo na kusema Nyoshi ameridhia kwa moyo mkunjufu.

Kelvin amesema mbali ya Nyoshi kuachia cheo hicho na kubakia kama mwanamuziki wa kawaida, lakini atakuwa mshauri wa bendi pale uzoefu wake utakapohitajika.

Kikao kilichomwondoa Nyoshi kwenye urais wa bendi kilifanyika jana katika ukumbi wa New Msasani Club, jijini Dar es Salaam ambapo menejimenti ya FM Academia ilitangaza mabadiliko hayo.

“Hakukuwa na utaratibu wa kupiga kura kama zinavyofanya baadhi ya bendi, bali menejimenti ilikuja na mependekezo yake na yakakubaliwa na mwanamuziki wote bila mtafaruku wowote,” alisema Kelvin Mkinga.

No comments