GIGGS AMTABIRIA POGBA "UFALME" OLD TRAFFORD

WINGA teleza wa zamani wa mashetani wekundu wa Old Trafford, Ryan Giggs ameweka bayana imani aliyonayo kwa kiungo Paul Pogba na kusema atakuwa “mfalme” mpya katika kikosi cha Manchester United msimu ujao.

Gigs ambaye kwa sasa ni kocha, aliyasema hayo katika mahojiano maalum ambapo alizungumzia baadhi ya masuala mbalimbali ikiwemo mwelekeo wa baadhi ya wanandinga wa Ligi ya premier.

Katika anachokiamini kocha huyo aliyewahi kuwa msaidizi wa Louis Van Gaal ndani ya kikosi cha United kabla ya kutua kwa Jose Mourinho, alisema Pogba ana nafasi kubwa ya kuwa katika kiwango kikubwa msimu ujao hivyo atabeba heshima kubwa kama alivyokuwa Wayne Rooney na Zlatan Ibrahimovic.

Alisema anaamini hivyo kwa sababu alianza kuonyesha thamani yake katika mechi muhimu za kabla ya kufungwa kwa msimu uliopita wa premier na hata kuisaidia United kutwaa uchampioni wa Kombe la Ulaya.

Akinukuliwa, Giggs alisema: “Nina uhakika msimu ujao utakuwa bora kwa mashabiki wa United kuona kiwango halisi cha Paul Pogba kwani atakuwa kwenye ubora zaidi.”

“Amekuwa akipandisha kiwango kadri siku zinavyokwenda tangu katika mechi za mwishoni mwa Ligi ya premier, hata sasa ni kati ya wachezaji walioifanya United kutwaa ubingwa wa Europa.”


“Amechangia kutwaa taji hilo na kisha kuifanya United kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya, hatua ambayo inamweka Pogba katika matumaini ya kung’ara zaidi msimu ujao,” alisisitiza Giggs ambaye kwa sasa ni kati ya wachambuzi wa soka.

No comments