GUARDIOLA ATETEA UFUJAJI WAKE WA FEDHA KWENYE USAJILI

INGAWAJE wataalamu wa soka wanasema kwamba anachofanya kocha wa Manchester City, Pep Guardiola ni kama fujo katika kumwaga fedha ovyo kwenye usajili, lakini yeye mwenyewe amejitetea.

Akihojiwa juzi baada ya malalamiko ya baadhi ya mashabiki kwamba kiasi cha fedha anachotoa ni kikubwa kwa baadhi ya wachezaji, kocha huyo amesema kwamba anachofanya ni kutokurejea makosa ya msimu uliopita.

“Tumemaliza msimu tukiwa katika nafasi ambayo haikuwa malengo yetu. Tunafanya usajili ambao malengo yake ni kutufikisha kwenye ubingwa,” amesema kocha huyo.

Baada ya msimu wa Ligi kumalizika, kocha huyo alitembeza panga kwenye kikosi cha Manchester City na wachezaji kadhaa kuonyeshwa mlango wa kutokea.

Baada ya dirisha la usajili tu kuanza, Guardiola akawapiga bao Real Madrid na Manchester United klwa kumnunua kiungo wa Monaco, Bernardo Silva kwa dau la pauni mil 43.

Baada ya kumnunua Bernaro Silva, siku kadhaa baadae ndani ya wiki moja, Guardiola akahamia kwa golikipa wa Benifica ya Ureno, Ederson ambapo anatarajia kuwa golikipa ghali katika ulimwengu huu wa soka.

Guardiola amepewa jina jipya la “Mr. Cheque book” ambalo amepewa siku za hivi karibuni kutokana na pesa anazomwaga tu kwa kila mchezaji ambaye anamtaka.

Wakati suala la golikipa Ederson likikamilika, tayari habari mpya kutoka familia ya mwanasoka anayekipiga katika klabu ya Monaco, Benjamin Mendy amekubali kujiunga na klabu ya Manchester City.

Picha za Mendy akiwa kwenye ndege binafsi siku ya Jumapili inahisiwa alikuwa akienda Uingereza ili kukamilisha taratibu za mwisho za usajili wake kwenda Manchester City.

“Kuna watu wanalalamika pia kwamba kwanini namnunua kipa kwa bei mbaya. Nawashangaa sana kwasababu kipa bora anakuhakikishia ulinzi imara katika timu yako,” alisema.


Amesema dhana kwamba makipa hawauzwi kwa bei mbaya imepitwa na wakati kwa sababu kuna makipa wengine ndio huchangia kuamua matokeo ya ubingwa.

No comments