HARUNA NIYONZIMA ASEMA BADO ANA IMANI NA YANGA... atamani mkataba mwingine msimu ujao

KIUNGO wa Yanga, Haruna Niyonzima amesema kwamba bado ana nafasi ya kuichezea Yanga iwapo watampa mkataba mwingine.

Niyonzima mkataba wake wa sasa unatarajia kumalizika mwezi ujao, huku kukiwa na uvumi kwamba anatakiwa na klabu kadhaa lakini yeye mwenyewe ameweka wazi kwamba Yanga ndio timu yake ya kwanza.

“Mkataba wangu unatarajia kumalizika mwezi ujao na mara baada ya kumalizika nitawapa nafasi kwanza klabu yangu ninayoichezea kabla ya kuchukua maamuzi mengine ya kusaini timu nyingine, mimi nipo Rwanda na mara nitaporudi nitaweka wazi kila kitu,” alisema.

Aidha, Niyonzima alisema kwamba tetesi zilizozagaa kwenye vyombo vya habari kwamba anatakiwa na klabu ya Simba si za kweli, kwani yeye bado hajamalizana na Yanga.

“Hizo ni tetesi za usajili, siwezi kuficha kitu chochote, bado sijafanya mazungumzo na Simba, mimi bado mchezaji halali wa Yanga.”

Hali hiyo imefanya awe anahusishwa na kujiunga na timu kadhaa na hasa watani wa Yanga, Simba.


Hii imekuwa kila unapokaribia usajili mpya lakini safari hii Niyonzima mwenyewe ameamua kuelezea kuwa anaiheshimu Yanga kwani imemtoa mbali kimaisha hivyo hawezi kukurupuka kipindi hiki cha usajili.

No comments