IBRAHIMOVIC KUREJEA KIKOSINI MAN UNITED MAPEMA

STRAIKA Zlatan huenda akarejea mapema kwenye kikosi cha Manchester United tofauti na inavyotarajiwa, baada ya staa huyo raia wa Sweden kusema kuwa atakuwa fiti ndani ya miezi mitano.

Gazeti la The Sun liliripoti kuwa licha ya staa huyo kuruhusiwa na klabu hiyo majira haya ya joto kutokana na majeraha ya goti, lakini amekuwa akijifua kwenye viwanja vya mazoezi vya Carrington.

Mbali na gazeti hilo, gazeti lingine  la Daily Star liliripoti kuwa Ibrahimovic anaweza kurejea uwanjani ndani ya kipindi hicho cha miezi mitano akiwa na kikosi hicho cha Manchester United.

Gazeti hilo lilieleza amekuwa akienda kwenye viwanja vya mazoezi vya man United vilivyopo barabara ya Littleton ili kuwashuhudia wanawe Maximillian na Vincent nao wakijifua.

“Kuna taarifa kwamba amewaeleza marafiki zake kuwa atakuwa fiti ndani ya miezi mitano na hivyo hatarajii kurejea uwanjani mwanzoni mwa mwaka ujao,” liliripoti gazeti hilo.

“Na endapo ataweza kupona upasuaji wake wa goti kwa haraka, haitawashangaza wengi kama man United watampa nafasi,” liliongeza gazeti hilo.


Msimu uliopita staa huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Sweden aliifungia timu hiyo mabao 28 na amekuwa akiruhusiwa kutumia viwanja hivyo vya Carrington wakati akiendelea kuwa chini ya uangalizi.

No comments