JAMES KOTEI, IBRAHIM AJIB NA SAID NDEMLA WAIVUTIA EVERTON

MSAFARA wa klabu ya Everton ya England upo jijini takriban juma moja sasa kwa ajili ya ziara ya kisoka, wakiwa wageni wa kampuni ya michezo ya kubahatisha ya Sportpesa ambapo taarifa za ndani zinasema kuwa wamenogewa na baadhi ya wachezaji wa Simba akiwemo James Kotei.

Sportpesa ambayo imezidhamini timu tatu za Simba, Yanga na Singida United inawakilishwa na baadhi ya watendaji akiwemo nahodha wa zamani wa Everton, Leon Osman.

Chanzo cha habari cha ndani ya klabu ya Simba zimeimegea saluti5 kuwa pamoja na kuja kuratibu ujio wa timu ya Everton nchini Tanzania, pia ina fursa ya kubaini vipaji vilivyoko nchini.

Imebainika kuwa msafara huo una taarifa nyingi kutoka ndani ya klabu ya Simba, hasa hatua yao ya kuibua vipaji na kuwa na utayari wa kuruhusu wachezaji wao kwenda kucheza soka la kulipwa, sera ambayo imeungwa mkono na wakongwe hao wa Ligi ya England.

Taarifa ambayo saluti5 inayo imesema kuwa mmoja wa wakala wa kuuza wachezaji ameitonya Simba kuwa baadhi ya wachezaji wa timu hiyo ya Mtaa Msimbazi huenda wakafaidika na ujio wa Everton akiwemo Kotei aliyeonyesha kiwango kikubwa katika mchezo wa fainali wa Kombe la Shirikisho uliopigwa mjini Dodoma.

Chanzo chetu kimebainisha kuwa, pamoja na Kotei aliyeibuka kuwa mchezaji bora katika mechi hiyo ambayo Simba iliibanjua Mbao FC mabao 2-1 na kutwaa ubingwa wa Shirikisho, pia wawakilishi wa Everton wamewaulizia wachezaji wawili ambao ni Ibrahim Ajib na Said Ndemla.


“Hawa jamaa kumbe walikuwa wanafuatilia mechi ya fainali ya Shirikisho na wamevutiwa na wachezaji watatu wa Simba ambao ni Kotei, Ajib na Ndemla ila hawajasema kama wana mpango gani nao,” kilieleza chanzo chetu.

No comments