JONAS MKUDE ASEMA ANA FURAHA KUONGEZA MKATABA SIMBA SC

BAADA ya kusaini mkataba mpya wa kuendelea kuichezea Simba, kiungo na nahodha wa Simba, Jonas Mkude amesema sasa ana furaha ndani ya timu hiyo.   

Mkude ambaye hivi karibuni aliongeza mkataba wa miaka miwili ya kuichezea timu ya Simba, aliibukia kikosi cha pili cha timu hiyo mwaka 2011 kabla ya kupandishwa kikosi cha kwanza mwaka 2012 na tangu mwaka 2013 amekuwa mchezaji muhimu wa kikosi cha kwanza cha wekundu hao wa Msimbazi.

Akiongea na saluti5, Mkude alisema kuwa alipogoma kusaini mkataba mpya si kwamba haipendi Simba bali alihitaji kuongezewa maslahi ili aweze kumudu gharama za maisha.

“Mpira ndio kazi yangu, hivyo huwezi kufanya kazi ambayo haina maslahi ukizingatia mimi nautegemea wenyewe ili kuendesha maisha lakini nawashukuru viongozi wangu tumezungumza na tumeelewana na mimi nimeongeza mkataba wa miaka miwili,” alisema Mkude.

Kiungo huyo mkabaji alisema mapumziko yake kwa sasa yatakwenda vizuri kwa sababu anajua tayari timu gani atachezea msimu ujao.

Mkude alisema, kuongeza mkataba mwingine Simba ni changamoto nyingine kwake kwani anatakiwa kudhihirisha ubora wake kwa kucheza kikosi cha kwanza na kuisaidia timu iweze kufikia malengo.


Mkude aliongeza kuwa, timu yao msimu ujao ina mabadiliko makubwa sana hivyo atalazimika ajifue vilivyo ili mchango wake kama nahodha uweze kuonekana.

No comments