JUMA ABDUL ADUWAZWA NA "UZUSHI" WA KUWA MBIONI KUHAMIA AZAM FC

BEKI wa Yanga Juma Abdul ameshangazwa na taarifa za kwamba yuko katika harakati za kuhamia Azam akisema kuwa yeye bado mali ya Yanga kwa mwaka mzima uliobaki katika mkataba wake.

Akiongea na saluti5, Abdul alisema taarifa za watu kuvumisha kwamba anahama Yanga zimekuja kufuatia hivi karibuni kuandika maneno “deal done” akimaanisha mambo yamekamilika, maneno ambayo yamewachanganya mashabiki mbalimbali wa Yanga.

Abdul alisema kwa sasa hana ofa ya kutimkia Azam na badala yake anachokiangalia ni kuitumikia klabu yake hiyo katika mkataba ulioko na kuwataka wana Yanga kutulia.

Alisema, bado ana furaha kubwa kubaki katika timu hiyo ambapo sasa anajipanga kusubiri maandalizi ya msimu mpya mara baada ya kurejea kwa kocha wao George Lwandamina.


“Unajua watu wamechukulia vibaya yale niliyoyaandika, mimi bado ni mchezaji halali wa Yanga na kwamba Azam waliwahi kunihitaji lakini sio sasa, niwahakikishie wana Yanga kuwa nitakuwepo msimu ujao,” alisema Abdul.

No comments