KAMATI YA UTENDAJI SIMBA KUKUTANA KUMJADILI MUSSA HASSAN MGOSI

KAMATI ya utendaji ya klabu ya Simba inatarajia kukutana kwa lengo la kumjadili meneja wao, Mussa Hassan Mgosi na kocha wa makipa, Abdul Salim.

Wawili hao walikuwa na mchango kwa Simba kuchukua ubingwa wa Kombe la Shirikisho katika msimu uliomalizika, baada ya kuifunga Mbao FC mabao 2-1 katika mchezo wa fainali uliochezwa uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.

Habari zilizopatikana ndani ya klabu hiyo zilieleza kwamba kamati ya utendaji imepanga kukutana kwa lengo ya kuboresha kikosi chao cha benchi la ufundi linaloongozwa na Joseph Omog.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, kamati hiyo ilishindwa kukutana jana kutokana na rais wa klabu hiyo, Evans Aveva na makamu wake, Geofrey Nyange “Kaburu” kushikiliwa na taasisi ya kupambana na kuzuia rushwa Tanzania (TAKUKURU), ambao wamefikishwa mahakamani kwa tuhuma zinazowakabili.

Viongozi hao wawili wa Simba walifikishwa jana katika mahakama ya hakimu mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam pamoja na maafisa wengine wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).


Kamati hiyo inatarajia kukutana kujadili nafasi hizo mbili baada ya viongozi hao kumaliza matatizo yao yanayowakabili kwa sasa.

No comments