KASEJA AMMIMINIA SIFA MECKY MAXIME... asema ni kocha bora zaidi kuwahi kufanya nae kazi

KIPA mkongwe wa timu ya Kagera Sugar, Juma Kaseja amepongeza uwezo wa kocha wake, Mecky Maxime ambaye aliwahi kuifundisha Mtibwa Sugar ya mkoani Morogoro.
Kaseja amewahi kucheza sambamba na kocha huyo kwenye kikosi cha timu ya Taifa Stars kabla ya Maxime kutangaza kustaafu na kugeukia fani ya ukocha.

“Nimekaa na makocha wengi wazawa nawafahamu lakini Maxime ni kocha bora zaidi kuwahi kufanya nae kazi. Ni mtu mwelewa na mwenye uwezo wa kumjenga mchezaji kisaikolojia,” alisema Kaseja.

“Siku aliponipigia simu nijiunge na Kagera wala sikusita kwasababu nilijua naenda kufanya kazi chini ya kocha mwelewa na wala haikuwa tatizo kwangu kusaini mkataba,” aliongeza kipa huyo.

“Nimepata tetesi kuwa anataka kuondoka Kagera Sugar na kama akiondoka nitajiuliza mara mbili kusaini mkataba mwingine.”

Pia kipa huyo alipoulizwa swali ni kocha gani wa kigeni aliyevutiwa nae, alimtaja Mzambia Patrick Phiri ambaye walikuwa wote kwenye klabu ya Simba.


“Patrick Phiri pia ni kocha mwingine ambaye nilifanya nae kazi katika mazingira mazuri, nae pia ni mwelewa na amenisaidia sana kunijenga kisaikolojia,” alimaliza.

No comments