KLOPP ATAMBA KUWA NA MPUNGA WA NGUVU KWA AJILI YA USAJILI UTAKAOIMARISHA KIKOSI CHAKE MSIMU UJAO

KOCHA wa Liverpool, Jurgen Klopp amesema kwamba anacho kitita cha kutosha kufanya usajili ambao utaimarisha kikosi chake msimu ujao wa Ligi.

Kocha huyo raia wa Ujerumani, amesema kwamba anajua kuwa kuna mashabiki wa timu yake wamesononeka sana, lakini “majembe” anayoleta msimu ujao yatawafanya wafurahi.

Klopp katika kuonyesha kwamba amepania kuonyesha makali yake, ameanza kuivuruga klabu ya Roma ya Italia ambapo amewaambia kwamba waseme wanachotaka lakini lazima amnyakue winga wao raia wa Misri, Mohamed Salah.

Klopp amesema anajua kwamba anatakiwa kuwa na uhakika wa kujenga kikosi imara na lazima atenge pesa ya uhakika pia kunyakua wachezaji ambao anawataka.

Amesema kwamba Salah ni mmoja wa wachezaji wa kiwango cha juu kabisa na katika umri wake wa miaka 24 amefanya makubwa katika Ligi Kuu ya Italia “serie A”.

Raia huyo wa Misri amepachika mabao 15 na kutengeneza mengine 11 katika msimu huu na kuisaidia timu yake kuwa katika moja ya timu za juu kwenye Ligi hiyo.

Salah si mgeni katika Ligi Kuu ya EPL kwani aliwahi kusajiliwa na Chelsea na akashindwa kuwika sana kisha akahamia kwenye miamba ya Italia, klabu ya Florentina na baadae Roma mwaka 2015.

Klopp amesema kwamba amevutiwa sana na nyota huyo na kwamba amewataka Roma kuweka makubaliano mezani ili kijana huyo aweze kuhamia kwa majogoo.


Ingawaje uhamisho huo haujatajwa utakamilika lini lakini Roma wamedaiwa kuwa wanataka kiasi cha pauni mil 25 kuachana na winga huyo.

No comments