KOCHA MPYA WA AS ROMA AWEKA HADHARANI 'SERA' ZAKE


EUSEBIO DI FRANCESCO aliyetambulishwa rasmi kuwa kocha wa AS Roma Jumatano,  ameahidi kutumia falsafa ya kushambulia aliyokuwa akiitumia tangu akiwa na timu ya Sassuolo aliyoipandisha Serie A mwaka 2013 na kuiwezesha kumaliza nafasi ya 12 msimu uliomalizika.

Kocha huyo aliyesaini mkataba wa miaka miwili kuifundisha timu hiyo aliyowahi kuichezea kwa mafanikio katika nafasi ya kiungo na kuisaidia kutwaa ubingwa wa Serie A msimu wa 2000-01, amechukua nafasi ya Luciano Spalletti, aliyejiuzulu mwisho wa msimu na kisha kupewa kibarua cha kuifundisha Inter Milan.

 “Ni wazi kufundisha katika klabu ndogo ni tofauti na kufundisha katika klabu kubwa na unaweza kubadilisha mbinu kwa sababu hiyo. Lakini hata nilipokuwa Sassuolo kamwe sikucheza soka ya kujihami dhidi ya yeyote... Tutacheza soka ya kushambulia na kujaribu kuwatawala wapinzani wetu,” alisema.


Roma iliyomaliza nafasi ya pili mara tatu katika misimu minne iliyopita, ipo katika harakati za kujaribu kumaliza utawala wa Juventus iliyoshinda taji la Serie A misimu sita mfululizo iliyopita.

No comments