KOCHA OMOG WA SIMBA AJINADI KUSUKA KIKOSI CHA KIMATAIFA ZAIDI

BAADA ya kupata uhakika wa kushiriki michuano ya kimataifa barani Afrika msimu ujao, kocha wa Simba, Joseph Omog amesema kwamba sasa anataka kusuka kikosi kitakachotisha Afrika nzima.

Omog ambaye ni raia wa Cameroon amesema kwamba katika msimu ambo umemalizika, yeye na msaidizi wake, Jackson Mayanja wamegundua mapungufu mengi katika kikosi chao lakini sasa wamepata muda wa kusuka Simba mpya.

Kocha huyo amesema kwamba amepanga kuitumia michuano ya Kombe la Sportpesa kwa ajili ya kukijenga zaidi kikosi chake kwa ajili ya msimu ujao.

Simba ambayo imemaliza msimu huu ikinyakua Kombe la FA, inatarajiwa kuwa na mapumziko ya takribani siku tano kabla ya kuanza kujiandaa na michuano hiyo.

Michuano hiyo itakayoshirikisha timu nane ambazo ni Simba, Yanga, Singida United na Jang’ombe Boys kutoka Tanzania na Tusker, Gor Mahia, Nakuru All Stars na AFC Leopard za Kenya, inatarajiwa kuanza kutimua vumbi Juni 5 mpaka 11 mwaka huu.

Omog amesema kuwa : “Tunashukuru tumemaliza msimu salama licha ya kuukosa ubingwa wa Ligi Kuu lakini kitendo cha kuchukua Kombe la FA ni faraja kubwa kwetu, hali ambayo itatufanya msimu ujao tujipange zaidi."

“Baada ya Ligi kumalizika kinafuata kipindi cha usajili ambapo hatukutakiwa kufanya makosa kwa hilo na hii michuano midogo ambayo tunakwenda kushiriki inaweza kutusaidia kuangalia wapi tunatakiwa tujiweke imara zaidi kabla ya kuanza kwa msimu ujao, lakini pia wale wachezaji waliokuwa wanakosa nafasi ya kucheza mara kwa mara wataanza kuonekana,” amesema kocha huyo. 

Lakini pia amesema kwamba watafanya usajili ambao utazingatia mahitaji ya timu na kwamba baadhi ya wachezaji ambao wameonyesha kiwango duni katika kikosi chake atawapa nafasi ya kuonyesha uwezo wao kwa mara nyingine katika michuano hiyo mipya.


Kocha huyo amesema kwamba anataka kusajili wachezaji wenye uwezo ambao wataitumikia Simba kwa mafanikio na kwamba kila anayewania kusajiliwa katika Simba lazima atambue kuwa Simba ijayo itakuwa na wachezaji wenye viwango vya juu kabisa.

No comments