KYLIAN MBAPPE ASEMA BADO ATAFAKARI KUBAKI MONACO AU KUSEPA


KYLIAN MBAPPE hajafunga mlango juu ya uwezekano wa kuondoka Monaco kiangazi hiki, licha ya klabu hiyo ya Ligue 1 kudai kuwa straika huyo kinda wa miaka 18 hatauzwa.

Kinda huyo raia wa Ufaransa ni mmoja wa nyota walioteka soko la usajili barani Ulaya, akifukuziwa na klabu kubwa kama Real Madrid, Manchester City, Man United na Arsenal.

Mbappe alianza kwa mara ya pili katika kikosi cha Ufaransa - Les Blues Jumanne usiku, na alipoulizwa kuhusu kujiunga na klabu nyingine kubwa barani Ulaya aliwaambia waandishi wa habari kuwa atakaa na familia yake akiwa mapumzikoni na watatafakari kitakachotokea.

“Ninakwenda nje na familia yangu na tutatafakari kuhusu nini kitatokea... tutaona pia kitakachotokea klabuni kwa sababu nina mkataba na klabu. Siko huru, lakini tutaona nini kitatokea,” alisema alipohojiwa baada ya mechi waliyoichapa England 3-2 ndani ya Stade de France.

Dili lolote kwa Mbappe linatarajiwa kugharimu karibu pauni milioni 130, hivyo kuandika rekodi mpya ya dunia katika usajili, huku Madrid ikiaminika kuwa karibu zaidi kunasa saini ya kinda huyo.

No comments