LEWIS MACHA ASEMA ANAKUJA SIMBA KUIPA MATAJI MAKUBWA ZAIDI

MSHAMBULIAJI wa zamani Kaizer Chief ya Afrika Kusini ambaye ni raia wa Zambia, Lewis Macha amesema anakuja Simba kuipa mataji makubwa zaidi.

Macha ambaye kwa sasa anacheza soka nchini Msumbiji katika klabu ya Ferroviario Maputo, amesema katika mahojiano na saluti5 kwamba kama mipango yake ya kusajiliwa Simba itakamilika basi wekundu hao watafurahia kazi yake.

“Kusema ukweli nimepata furaha ya ajabu kusikia kwamba Simba wananitaka, nimesikia kwamba viongozi wake wameshafanya mazungumzo na klabu yangu ya sasa lakini nikuhakikishie kwamba nakuja Tanzania kwa kazi moja tu ya kuipa Simba mafanikio katika Afrika,” amesema.

Macha amesema kwamba ameambiwa pia na aliyekuwa kocha wa Simba raia wa Zambia, Patrick Phiri kuwa Simba ni timu nzuri hivyo anataka kuja kuhakikisha anapambana na kuitumikia vyema klabu hiyo.

“Simba ni timu kubwa, naifatilia sana siku nyingi. Lakini nimeifuatilia zaidi wakati huu niliposikia kwamba natakiwa huko. Nimeangalia video zake na kutambua kuwa ina wachezaji wazuri pia,” amesema.


“Navutiwa sana na uchezaji wa beki wao wa kushoto, yule kijana mwenye umbo dogo (Mohammed Hussein), nasikia ndio amekuwa mchezaji bora wa msimu huko Tanzania. 
Ametulia na ningependa kufanya kazi nae,” amesema Macha.

No comments