LIGU KUU ENGLAND KUANZA AGOSTI 12 ...Chelsea kuanza na Burnley, Man United na West Ham


RATIBA ya msimu mpya wa Ligi Kuu England (Premier League) 2017/18 imetangazwa na msimu utaanza rasmi Agosti 12, huku mabingwa watetezi Chelsea wakiongozwa na Antonio Conte, wakianza nyumbani Stamford Bridge dhidi ya Burnley Agosti 12, ikiwa ni miezi mitatu baada ya kushinda taji kwa pointi saba zaidi mbele ya Tottenham.

Washindi wa pili, Tottenham wataanzia ugenini St James' Park kwa msimu wa saba mfululizo wakiwafuata Newcastle waliorudi Ligi Kuu msimu huu chini ya Rafa Benitez. Itakuwa ni marudio ya mechi yao ya ufunguzi wa msimu wa 2012/13, ambayo Spurs walilala 2-1.

Chelsea na Tottenham zitakutana uso kwa uso Wembley katika wiki ya pili ya msimu mpya wa Premier League.

Jose Mourinho na Manchester United yake wataanza na West Ham nyumbani Old Trafford, wakati majirani zao City chini ya Pep Guardiola watawafuata wageni wa ligi, Brighton.

Wageni wengine katika Premier League, Huddersfield, wataanzia nyumbani kwa Crystal Palace, huku mabingwa wa 2016 Leicester watawafuata Arsenal walio kwenye kibarua cha kujaribu kurudi Top Four wakati Liverpool ikisafiri hadi Watford.
Everton chini ya Ronald Koeman itakuwa na mwanzo mgumu kuliko klabu nyingine yoyote kwani baada ya kuanza na Stoke, itasafiri kuzifuata Manchester City na Chelsea, kabla kuikaribisha Tottenham na kisha kusafiri tena hadi Old Trafford kucheza na Manchester United.

Katika mechi nyingine za ufunguzi, Southampton itaivaa Swansea na West Brom itakuwa nyumbani dhidi ya Bournemouth.

Manchester na Merseyside derby zimepangwa kupigwa siku moja Desemba 9. Wakati Manchester City itakwenda Old Trafford, Everton itasafiri hadi Anfield. Marudiano ya mechi hizi pia yamepangwa siku moja - Aprili 7.

United itawavaa wapinzani wao wa jadi Liverpool Oktoba 14 Uwanja wa Anfield na watarudiana wakati vijana wa Mourinho watakapowaalika wenzao wa Jurgen Klopp ndani Theatre of Dreams Machi 10.

Macho yote yanatarajiwa kuelekezwa Arsenal msimu huu baada ya uamuzi wa Arsene Wenger kubaki Emirates na Mfaransa huyo kibarua chake kinaweza kuota nyasi wakati Gunners itakapokwenda Anfield kwa mechi ya tatu Agosti 26.

MECHI ZA UFUNGUZI
Arsenal v Leicester City
Brighton and Hove Albion v Manchester City
Chelsea v Burnley
Crystal Palace v Huddersfield Town
Everton v Stoke City
Manchester United v West Ham United
Newcastle United v Tottenham Hotspur
Southampton v Swansea City
Watford v Liverpool
West Bromwich Albion v Bournemouth

MECHI ZA MWISHO
Burnley v Bournemouth
Crystal Palace v West Bromwich Albion
Huddersfield Town v Arsenal
Liverpool v Brighton and Hove Albion
Manchester United v Watford
Newcastle United v Chelsea
Southampton v Manchester City
Swansea City v Stoke City
Tottenham Hotspur v Leicester City

West Ham United v Everton

No comments