LIPULI FC KUMALIZANA NA SELEMANI MATOLA LEO

UONGOZI wa Lipuli FC unatarajia kuingia mkataba mpya leo na kocha wa zamani wa Simba, Selemani Matola kwa ajili ya kuifundisha timu hiyo msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania bara.

Akiongea na saluti5, Katibu mkuu wa Lipuli FC, Willy Chikweo alisema mazungumzo kati yao yamekwenda vyema na wanatarajia kusaini mkataba leo ili Matola aanze kazi mapema kuelekea Ligi hiyo.

“Nashukuru mazungumzo yamekwenda vyema na tunatarajia leo tutasaini nae mkataba ili aanze kazi mara moja. Kama unavyojua, tuko kwenye usajili na tukimalizana nae zoezi la usajili litaanza mara moja,” alisema.

Kwa upande wa Matola, alisema kila kitu kimekwenda vyema na anachosubiri kwa sasa ni kuingia mkataba na timu hiyo ili aanze kazi mara moja.

“Kila kitu kimekwenda vizuri, nadhani baada ya kusaini mkataba nitaanza kazi yangu mara moja, kwasababu mpaka sasa zoezi la usajili kwenye kikosi cha Lipuli halijaanza,” alisema Matola.


Lipuli ni moja ya timu zilizopanda daraja msimu uliomalizika kutoka daraja la kwanza hadi Ligi Kuu ambapo msimu ujao itakuwa kati ya timu 16 zitakazocheza Ligi Kuu Tanzania bara.

No comments