LOWENDOWSKI ASEMA ANAITAMANI REAL MADRID LEO KESHO

STRAIKA wa mabingwa wa Bundesliga, Robert Lowendowski ameshindwa kuzuia hisia na ndoto alizonazo juu ya klabu ya Real Madrid na kuipa presha klabu yake ya Bayern Munich.

Mchana kweupe nyota huyo wa timu ya taifa ya Ujerumani ameweka bayana kuwa anatamani siku moja ajikute anavaa uzi wa Real Madrid tena chini ya kocha Zinedine Zidane.

Lakini taarifa za ndani ya mabingwa hao wa Bundesliga zinasema kuwa huenda straika huyo akaanza mazungumzo ya kurefusha mkataba hadi mwaka 2021.

Lowendowski kwa sasa anaitumikia Bayern Munich ndani ya kandarasi itakayomalizika mwishoni mwa msimu wa mwaka 2019.

Hata hivyo, Lowendowski hajaweka bayana hatma ya soka lake la baadae, ingawa kwa kauli yake ya sasa, kuna uwezekano mkubwa wa kuihama Bayern Munich pindi muda mwafaka utakapowadia.

Akizungumza na kunukuliwa na Sky Sports, Lowendowski alisema anatambua ubora wa timu na weledi wa kisoka wa kocha Zidane.

Alisema, pamoja na kutambua hilo, anaamini iko siku dili la kutua Madrid litafanikiwa ingawa hakutaja lini.


“Ninaamini katika mambo mengi, lakini moja la klabu ninayoota kuitumikia ni Real Madrid, hasa chini ya kocha Zidane,” alisema Lowendowski.

No comments