MAANDALIZI YA TIMU YA TAIFA YA MCHEZO WA MIELEKA BONGO KUANZA MWEZI HUU

CHAMA cha mchezo wa mieleka Tanzania (AWATA), kimesema kuwa timu ya taifa ya mchezo huo inatarajia kuanza maandalizi kwa ajili ya kushiriki mashindano ya kimataifa hivi karibuni.

Akiongea na saluti5, Katibu msaidizi wa AWATA, Eliakim Melckzedeck alisema kuwa timu hiyo inatarajia kuanza maandalizi ya kambi mwezi huu wa Juni.

Alisema kuwa tayari timu hiyo ipo na ilipatikana katika mashindano ya Muungano yaliyofanyika Zanzibar mwaka huu ambayo yalishirikisha timu kutoka Tanzania Bara na Visiwani.

Melckzedeck alisema kuwa maandalizi yanayofanyika hivi sasa ni kupata fedha pamojam na Kamati kuendelea kuangalia wachezaji ambao walionyesha uwezo kupitia mashindano ya ndani ya kitaifa, ili kuweza kuongeza idadi ya wachezaji.

Katibu huyo alisema kuwa chama kimejipanga kuhakikisha wachezaji wake wanaandaliwa vyema ili kwenda kufanya vizuri katika mashindano hayo ya kwanza kimataifa tangu chama hicho kifunguliwe.

“Kwa kweli sisi chama tuna shauku kubwa ya kuhakikisha timu yetu inashiriki mashindano ya kimataifa ambayo yapo mbele yetu hivi sasa, hivyo tunatarajia kuanza kambi mwezi huu kwa maandalizi zaidi,” alisema Melckzedeck.


Alitoa wito kwa wadau kuunga mkono na kusapoti timu hiyo ya taifa kwani ushindi utakaokwenda kupatikana utakuwa ni wa taifa ambao utaweza kuiletea heshima nchi yetu kwa ujumla. 

No comments