MANCHESTER CITY BADO YAKOMAA NA ALEXIS SANCHEZ


MANCHESTER CITY imeripotiwa kuzidi kupata uhakika kwamba Arsenal itashindwa kuhimili shinikizo na kuishia kumpiga bei Alexis Sanchez kiangazi hiki badala ya kumpoteza kwa uhamisho usio na malipo mwakani.

Staa huyo wa kimataifa wa Chile, amebakisha mwaka mmoja katika mkataba wake Emirates Stadium, na amekuwa akihusishwa na klabu kadhaa kubwa kiangazi hiki wakati Arsenal ikikabiliwa na mtanziko juu ya mustakabali wake.

Arsenal inapigana kumbakisha Sanchez kwa mwaka wa mwisho wa mkataba wake na kuwa tayari kumpoteza bure mwisho wa msimu au kumuuza kwa Bayern Munich kuliko kumruhusu kujiunga na wapinzani wao katika Premier League – Manchester City.

Bayern Munich inaripotiwa kutenga pauni milioni 40, lakini City inaamini kuwa inaweza kuishawishi Arsenal kwa kuongeza pauni milioni 10 zaidi na kuwaachia staa huyo amaye kwa upande wake yuko tayari kujiunga na miamba hiyo ya Etihad lakini si kwenda Ujerumani.

Arsenal haina rekodi nzuri linapokuja suala la kuzuia wachezaji wake nyota, na itakuwa katika wakati mgumu zaidi mwaka huu baada ya kushindwa kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya.

No comments