MANCHESTER UNITED YAIPIGA BAO REAL MADRID

KLABU ya Manchester United imewazidi kete Real Madrid na kuwa timu ya soka ya kwanza yenye thamani kubwa, kwa mujibu wa gazeti la biashara la Forbes.

Thamani ya United imekuwa dola bil 3.69 na imerudi kileleni katika orodha ya majumuisho ya mwisho ikiwa ni mara ya kwanza kwa kipindi cha miaka mitano.

Klabu ya Hispania, Barcelona imeshika nafasi ya pili ikiwa na thamani ya dola bil 3.64, huku Real ikiwa nafasi ya tatu kwa kuwa na thamani ya dola bil 3.58.

Timu sita za Uingereza ziko kwenye 10 bora, huku Manchester City, Arsenal, Chelsea, Liverpool na Tottenham zikiingia kwenye orodha hiyo.

Mabingwa wa Ujerumani, Bayern Munich wameshika nafasi nne wakati miamba ya Italia, Juventus ikishika nafasi ya tisa.

Real ambayo imeshinda taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya imekuwa nafasi ya kwanza kwa kipindi cha miaka minne mfululizo iliyopita, lakini sasa thamani yao imeshuka kwa asilimia mbili wakati United thamani yake imepanda kwa asilimia 11.

“Kurudi kwa Manchester United katika nafasi ya kwanza inamaanisha kwamba wana nguvu kubwa mno kwenye idara ya masoko na ni bidhaa yenye soko kubwa,” amesema naibu mhariri mtendaji wa Forbes Media, Mike Ozanian katika taarifa yake kwa waandishi wa habari.

Leicester City ambao walishinda taji la Ligi Kuu England msimu wa mwaka 2015/16 na Westham, zote ziko kwenye 20 bora.

No comments