MAURICIO PELLEGRINO ATAMBA KUIBADILI SOUTHAMPTON

BABA wa kazi katua mwanangu! Unaweza kusema hivyo kama wewe una ushabiki wa kudumu wa miamba wa Southampton ya Uingereza.

Baada ya kuachana na aliyekuwa kocha wao, Claude Puel ambaye alitemwa mapema mwezi huu, klabu hiyo inayocheza soka la kuvutia imeamua kumpa mkataba kocha mwenye mafanikio makubwa, Mauricio Pellegrino.

“Kwa aina yangu ya ufundishaji na jinsi ninavyoiona timu hii maana yake ni kwamba tutakuwa katika wakati bora kabisa,” amesema Pellegrino baada ya kulamba mkataba wa miaka mitatu ya kuinoa timu hiyo.

“Falsafa yangu mimi ni kwamba kila mechi tunatakiwa kushinda. Tutakuwa tunaingia uwanjani kwa kuwa na matumaini ya kushinda kila mechi hadi tuwe mabingwa,” alisema.

Makamu mwenyekiti wa Southampton, Lesreed amesema kwamba kocha huyo ambaye ni mlinzi wa zamani wa Liverpool anafahamika kwa ukali wake na jinsi anavyohimiza ushindi.

“Kama alikuwa anatafuta mahali pa kufanyia kazi yake kwa ufanisi zaidi basi St. Mary’s ni mahali mwafaka kwake kabisa,” amesema.

Pellegrino alikuwa anafanya kazi katika klabu za Independiente na Estudiantes nyumbani kwao Argentina kwa miezi saba baada ya kutupiwa virago na klabu ya Valencia.


Kabla ya kuwa katika miamba hao wa Hispania, kocha huyo amefanya kazi katika klabu ya Liverpool ambako aliwahi kuwa mchezaji chini ya kocha mkuu, Rafael Benitez kati ya mwaka 2008 na 2010 na baadae akawa na Inter Milan 2010.

No comments